Job 11
1Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu: 1
2“Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa? 2 Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki? 1
3Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya? 2 Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka? 1
4Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili 2 nami ni safi mbele zako.’ 1
5Aha! Laiti kwamba Mungu angesema, 2 kwamba angefungua midomo yake dhidi yako, 1
6naye akufunulie siri za hekima, 2 kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili. 2 Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako. 1
7“Je, waweza kujua siri za Mungu? 2 Je, waweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi? 1
8Ni juu mno kuliko mbingu: waweza kufanya nini? 2 Kina chake ni kirefu kuliko kuzimu: 2 wewe waweza kujua nini? 1
9Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia, 2 nacho ni kipana kuliko bahari. 1
10“Kama akija na kukufunga gerezani, 2 na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga? 1
11Hakika anawatambua watu wadanganyifu; 2 naye aonapo uovu, je, haangalii? 1
12Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima, 2 endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu. 1
13“Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake 2 na kumwinulia mikono yako, 1
14ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako 2 wala usiuruhusu uovu ukae hemani mwako, 1
15ndipo utainua uso wako bila aibu; 2 utasimama imara bila hofu. 1
16Hakika utaisahau taabu yako, 2 utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita. 1
17Maisha yako yatangʼaa kuliko adhuhuri, 2 nalo giza litakuwa kama alfajiri. 1
18Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini; 2 utatazama pande zote na kupumzika kwa salama. 1
19Utalala, wala hakuna atakayekuogofya, 2 naam, wengi watajipendekeza kwako. 1
20Bali macho ya waovu hayataona, 2 wokovu utawaepuka; 1 tarajio lao litakuwa ni hangaiko 2 la mtu anayekata roho.”